Home 2024 August 31 “MAUAJI” MATATU YA KIKATILI!

“MAUAJI” MATATU YA KIKATILI!

“MAUAJI” MATATU YA KIKATILI!

Kila mwanafunzi wa Neno la Mungu, anapaswa kujua mauaji matatu ya kikatili ambayo historia yote ya Kibiblia inazunguka. Mauaji haya matatu yanawakilisha mwitikio wa Israeli kwa mwito wa Mungu mara tatu wa kutubu. Mauaji hayo, yanaeleza dhambi isiyosamehewa na kutengeneza USULI wa kipindi cha sasa cha neema.

Ilikuwa ni Yohana Mbatizaji, nabii wa mwisho wa Agano la Kale, ambaye alitumwa kama Eliya (Mathayo 17:10-13), mtangulizi wa Kristo, kuwaita Israeli watubu. Alikatwa kichwa na Herode, “mfalme wa Wayahudi” mwovu na mchafu. Baada ya Yohana, Kristo mwenyewe alichukua kilio cha Yohana Mbatizaji: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia“. Yeye naye, walimsulubisha – akauwawa! Kisha, wakati wa Pentekoste, Israeli walipewa nafasi ya tatu ya kutubu, mpaka walipomwaga damu tena, wakampiga Stefano kwa mawe hadi kufa.

Ikumbukwe pia kwamba, hatia yao, pamoja na uadui wao mkali, viliongezeka katika mauaji ya pili na ya tatu! Kama Israeli, wangeitikia mwito wa Yohana Mbatizaji wa kutubu, Herode hangethubutu kamwe kumtia Yohana Mbatizaji gerezani. Hii pia, inaeleza ni kwa nini Bwana wetu hakufanya chochote ili kumsaidia Yohana Mbatizaji aweze kuachiliwa kutoka gerezani, ingawa jambo hilo lilikuwa limemchukiza Yohana. Hilo, halikuwa lake yeye Kristo, bali lilikuwa ni la Israeli, ambao walitakiwa wafanye jambo fulani kuhusu kifungo hicho kisicho cha haki cha Yohana Mbatizaji na kila dakika moja aliyokaa gerezani ilikuwa ni ushuhuda dhidi yao. Soma kwa makini Luka 3:18-20; Luka 7:19-29; na Mathayo 14:1-11.

Ndiyo Kusema, juu ya kukatwa kichwa kwa Yohana Mbatizaji, Israeli waliruhusu! Juu ya kusulubishwa kwa Kristo, Israeli walidai (Luka23:23-24). Na juu ya kupigwa kwa mawe kwa Stefano, Israeli walifanya wenyewe, wakamtoa nje ya mji kwa mikono yao wenyewe na kumpiga mawe huko…

Na hivi ndivyo, kizazi hicho katika Israeli, kilifanya ile dhambi isiyoweza kusamehewa ambayo Bwana wetu alionya kwamba haitasamehewa, ama katika enzi hiyo, au katika enzi zijazo. Kwa sababu hiyo, tunahitimisha andishi hili kwa kunukuu vifungu vyenye thamani kuu kutoka kwenye nyaraka za Mtume Paulo ambazo zinakataa, kwa uwazi, uwezekano wowote wa kuwepo wa “dhambi yoyote isiyosameheka” wakati huu wa “maongozi ya neema ya Mungu” ya sasa:

“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake” (Waefeso 1:7)

“Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; na dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi; ili kwamba, kama vile dhambi ilivyotawala katika mauti, vivyo hivyo kwa njia ya haki neema itawale hata uzima wa milele kwa Yesu Kristo Bwana wetu.” (Warumi 5:20-21)

Utukufu una Yeye KRISTO YESU Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *