Home 2024 June 04 KUMFUATA YESU KATIKA MWILI!

KUMFUATA YESU KATIKA MWILI!

KUMFUATA YESU KATIKA MWILI!

Watu wengi wa “kidini” humchukulia Bwana Yesu Kristo kama kielelezo chao katika maisha yao ya “U-Kristo”. Wanamwita “Mfano Mkuu”. Wakristo hao wakipatwa na tatizo lolote lile, hujiuliza: Je! Katika tatizo hili, “Yesu angefanya nini?” Wakristo hawa, wanautafuta wokovu wao kwa “kutembea katika hatua za Yesu”.

Ingawa wema na maadili ya kiroho ya Bwana wetu yanastahili kuigwa, lakini kulikuwa na mambo mengi katika mwenendo Wake ambayo hatuwezi kuyaiga, aslani! Kwa mfano, hakuna hata mtu mmoja miongoni mwetu leo ambaye anaweza kuwa katika nafasi ya “kuwatangazia” wanafiki, unafiki wao, (hasa wale wa kidini) na kuwakemea kwa mamlaka kama ambavyo Bwana wetu aliwatamkia Mafarisayo wa siku zake – kwa sababu tu, sisi sote, tuna U-farisayo mwingi ndani yetu.

Hata hivyo, hakika hatuwezi kuokolewa kwa “kumfuata Kristo,” au “kujitahidi kuishi kama Yeye alivyokuwa akiishi”. UTAKATIFU WAKE MKAMILIFU, UNGETHIBITISHA TU UDHALIMU WETU NA KUTUHUKUMU. Zaidi sana, Yeye alikuja kutuokoa, si kwa uhai wake, bali kwa kifo chake; Ndio maana, “KRISTO ALIKUFA KWA AJILI YA DHAMBI ZETU” (1 Wakorintho15:3), na wenye dhambi “WAMEPATANISHWA NA MUNGU KWA MAUTI YA MWANA WAKE” (Warumi 5:10).

Lakini Mungu ametupa kielelezo cha “kukifuata” katika wokovu wetu. Ni Sauli wa Tarso, aliyekuja kuwa Mtume Paulo, mkuu wa wenye dhambi waliookolewa kwa neema. Hiki ndicho anachosema, kwa maongozi ya Roho wa Mungu:

“NI NENO LA KUAMINIWA, TENA LASTAHILI KUKUBALIKA KABISA, YA KWAMBA KRISTO YESU ALIKUJA ULIMWENGUNI ILI AWAOKOE WENYE DHAMBI; AMBAO WA KWANZA WAO NI MIMI” (1 Timotheo 1:15)

Kumbuka, Mtume Paulo, akiwa Sauli wa Tarso, alikuwa anakiliongoza taifa lake la Israeli na ulimwengu katika uasi dhidi ya Mungu na Kristo Wake; huku “akiwaonea hasira kama mwenye wazimu” wanafunzi wa Kristo (Matendo 26:11) na huku “akiwatisha na kutishia kuwaua” wanafunzi hao (Matendo 9:1). Lakini, pamoja na mabaya hayo ya Sauli wa Tarso, ni Kwa nini basi, Mungu alimwokoa mtu kama huyu? Yeye mwenyewe, anaendelea kutuambia maneno haya katika aya inayofuata:

“LAKINI KWA AJILI HII NALIPATA REHEMA, ILI KATIKA MIMI WA KWANZA, YESU KRISTO AUDHIHIRISHE UVUMILIVU WAKE WOTE, NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE, WAPATE UZIMA WA MILELE” (Mstari wa 16)

Je! Kuna FUNZO lolote katika hili???

Nakushauri, chukua hatua na kufuata msimamo wako na Mtume Paulo; Kwamba Kubali kuwa wewe ni mwenye dhambi na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, ATAKUOKOA!!!

Utukufu una Yeye KRISTO YESU Milele na Milele AMINA

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *