TUNDA LA NEEMA YA MUNGU
Wakati ule Yohana Mbatizaji na Bwana wetu Yesu Kristo walipotokea duniani, watu wa Mungu (Israeli) walikuwa chini ya Sheria ya Musa kwa takribani miaka elfu moja mia tano hivi. Ni ajabu kidogo kuona kwamba Yohana na Bwana wake bado walitafuta ‘matunda mema’ kati yao.
Wakati viongozi wa kidini wanafiki wa wakati huo walipokuja kujiunga na hadhira iliyokua ya Yohana na kuomba kubatizwa naye, Yohana Mbatizaji aliwaita “kizazi cha nyoka” na kuwaambia “wazae matunda yapasayo toba” (Mathayo 3:7-8). Toba ya kweli, yenye matunda ya kuithibitisha; ilikuwa hitaji la msingi la ufalme aliotangaza Yohana Mbatizaji. Hili linadhihirika kutokana na tamko lake:
“Na sasa shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti, kwa hiyo kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni” (Mathayo 3:10).
Bwana wetu Yesu alitokea, akitangaza ujumbe sawa na wa Yohana Mbatizaji, naye pia akatafuta matunda mema kati ya watu wake (Mathayo 7:16-20; 21:33-43). Tunajua, hata hivyo, kwamba Yohana Mbatizaji alikatwa kichwa na Kristo Yesu alisulubiwa. Matunda yaliyopatikana, chini ya Sheria, yalikuwa ni machache kweli kweli au pengine hayakuwepo kabisa! Hata baada ya ufufuo wa Kristo, wengi wa watu wake, walikataa kutubu na kushindwa kuzaa matunda yaliyotakiwa.
Lakini, kile ambacho Sheria ya Musa ilikuwa inakihitaji, Neema ya Mungu ilikitoa! Ilikuwa ni wakati huu ambapo Mungu alimwinua Mtume Paulo, ambaye “mahubiri yake ya msalaba” yalionyesha kwamba Kristo hakufa kifo cha ghafla, bali kwa upendo usio na kipimo, alikuja ulimwenguni kufa kwa ajili ya wenye dhambi ili waokolewe kwa neema, kwa njia ya imani (Waefeso 2:8-9). Ujumbe wa Paulo uliitwa “injili [habari njema] ya neema ya Mungu” (Matendo 20:24), na pale ambapo Sheria ilishindwa kuzaa matunda, neema ilileta (ilizaa) matunda hayo kwa wingi.
Neema ya Mungu katika Kristo, inapokubaliwa katika imani ya kweli, daima huzaa matunda mema. Hivyo Mtume Paulo aliwaandikia Wakolosai kwamba habari njema yake ilikuwa ikienea katika ulimwengu wote, akiongeza: “na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokuwa kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli” (Wakolosai 1:5-6).
Kubali ujumbe wa Mungu wa neema yake, mwamini Kristo kama Mwokozi wako na yeye atakusaidia kuzaa matunda mengi mema.
Utukufu una Yeye KRISTO Milele na Milele AMINA
Leave a Reply