Home 2020 November 26 JE! TUNAMTUKUZA PAULO?

JE! TUNAMTUKUZA PAULO?

JE! TUNAMTUKUZA PAULO?

“Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.” (2 Wakorintho 12:7)

Mara nyingi tukiwa tukiongea na wahudumu wa kikristo waliokata tamaa kutokana na changamoto mbalimbali, na kuwaambia juu ya utume wa Paulo na jinsi nyaraka zake zilivyokuwa na maneno mazuri ya kuwatia moyo hivyo wazisome nazo zitawapa faraja na kuwafanya wachangamke. Jibu lao linakuwa, “Ndio, lakini yapo mambo mengi kwenye Biblia kuliko Paulo!” Majibu yetu kwao huwa, “Ni kweli, lakini nyaraka za Paulo ni Neno la Mungu kwao kama watu wa Mataifa wanaoishi katika majira ya uachilio wa Neema ya Mungu.” Wapendwa hawa, mara zote, hushikwa na butwaa katika mwonekano wa sura zao; kwa sababu walikuwa hawajawahi kusikia ukweli huu ulio wazi wa Biblia yetu! Ikiwa unataka kujua leo ni nini Mungu anasema na wewe, ni lazima usome nyaraka za mtume Paulo, yaani Warumi mpaka Filemoni. Nje ya hizo, Kila kitu kingine kilichopo katika Biblia ni Neno la Mungu kwa Israeli, na wewe sio Israeli!

Unalazimika kumtenganisha Mtume Paulo na mitume wengine wote kwenye Biblia. Kama Kanisa lako na Mchungaji wako hawafanyi hivyo, una chaguo la kufanya – la kumtii Mungu, au kuwatii wanadamu. Lakini ni nini hasa kinachomfanya Mtume Paulo kuwa ni wa kipekee? Katika Injili Nne, tunamwona Bwana Yesu Kristo akiwapa mitume wake kumi na wawili amri iliyo wazi (Mathayo 10:5-6):

“Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.”

Na Yesu aliendelea katika aya ya 40, “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.”

Bwana Yesu Kristo alimtuma Petro na wale kumi na mmoja kuhudumia taifa la Israeli (kwa bahati mbaya, washiriki wengi wa kanisa hawajawahi kufundishwa ukweli huu rahisi). Yesu aliwaambia kwamba ikiwa hakuna mtu anayetaka kuwapokea, mtu huyo alikuwa akimkataa Yeye (Yesu Kristo), na kwa kufanya hivyo anamkataa Mungu Baba aliyemtuma. Swali sasa linabaki kuwa: “Je! Ni nani Yesu Kristo alituma kwetu sisi watu wa Mataifa?” Hakika hakuwa Petro na wala wale kumi na mmoja kwa sababu walikuwa na huduma yao kati ya Wayahudi, taifa la Israeli. Wagalatia 2:9 inasema kwamba Petro, Yakobo, na Yohana ni mitume wa Israeli (tazama pia Mathayo 19:27-28).

Angalia Warumi 11:13, ambapo Mtume Paulo anaandika: “Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu.” Ni nani mtume wa Mungu wa Mataifa? PAULO! Bwana Yesu Kristo aliyepaa, baada ya kufufuka, alimchagua Paulo kuwa mtume wa Mataifa.

Katika Matendo 9:15-16, Bwana Yesu alimwambia Anania:

“Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.”

Paulo aliandika katika Warumi 15:16:

“Ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.”

Na katika Wagalatia 1:16 ameandika:

Alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu.”

Mwishowe katika 2 Timotheo 1:11 ameandika:

“Ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu wa watu wa Mataifa.”

Mtume Paulo ni mtume wetu; ndiye Mungu aliyemtuma kwetu. Paulo ni msemaji wa Mungu kwetu leo. Kwa hivyo, ikiwa tunapuuza Paulo – kama vile wengi wanaodai kuwa ni Wakristo wanavyofanya leo – kwa kweli tunampuuza Mungu na Neno Lake kwetu sisi Mataifa katika kipindi hiki, cha majira ya uachilio wa Neema!

Ebu angalia 2 Petro 3:15-16, moja ya kauli za mwisho (WOSIA) wa Mtume Petro, ambaye aliandika maneno haya:

“Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.”

Je! Umeona kile Petro alichoandika? Alisisitiza juu ya nyaraka za Paulo! Hapa unamwoma Petro, mmoja wa mitume wakuu wa Israeli, akihimiza kusomwa nyaraka za Paulo. Je! Watu wataweza kusema “Mtume Petro alimtukuza sana Mtume Paulo?” Hapana, kamwe! Katika jambo hilo, hawana haki ya kusema kwamba “tunamtukuza sana Paulo,” hata kidogo. Hizi ni tuhuma tu za uwongo katika ujinga, zilizoundwa na kuenezwa na wakosoaji wetu, wanaopatikana katika sheria na mapokeo ya dini, ambao wamedhamiria kudharau msimamo wetu ili waweze kushikilia na kuziishi mila za kanisa/dhehebu lao.

Hatumfanyi Mtume Paulo kuwa mungu; wala mtume Paulo sio Mungu, lakini Mungu ndiye amemtuma kwetu na kwa hiyo ingekuwa ni bora zaidi kwetu sisi kuusikiliza ujumbe ambao Mtume Paulo amepewa na Mungu atuletee. Tunatakiwa tutambue kwamba nyaraka za Mtume Paulo kuwa ni Neno la Mungu kwetu. Tunajifunza katika vitabu vyote 66 vya Biblia, lakini vitabu visivyo vya Mtume Paulo ni vya masomo ya kimsingi, ingawa havijaandikwa kwetu au juu yetu. Nyaraka zisizo za Paulo katika Biblia haziwezi kutumika kwetu wakati wote. Mtume Paulo alikuwa mtu kama sisi, lakini hakuandika fikra zake au maoni yake yeye mwenyewe binafsi. Kwa kadiri Roho wa Mungu alivyomwongoza, aliandika mafundisho ya neema yaliyoandikiwa Kanisa, Mwili wa Kristo. Yeye ni mwandishi pekee wa Biblia aliyewaandikia watu wasio Waisraeli ambao wanaishi nje ya kusudi la Mungu na mpango wake kwa Israeli (Warumi 16:25, 26; Waefeso 3:1-9). Mahusiano ya sasa ya Mungu na mwanadamu yanapatikana tu katika nyaraka za Mtume Paulo. Tunasisitiza juu ya wadhifa (ofisi/huduma) ya mtume wa Mataifa, na sio mtu anayeitwa Paulo. Kama vile Wayahudi walivyomtegemea Musa awape mafunuo ya Mungu, vivyo hivyo nasi leo, tunategemea nyaraka za Paulo kupokea mafunuo ya Mungu kwetu.

Katika uhalisia wake, wale wanaoamini kuwa Kanisa (Mwili wa Kristo) lilianza kwa huduma ya Paulo, “hawamtukuzi sana Paulo” – bali Mungu Roho Mtakatifu, katika Biblia ndiye “anamfanya hivyo Paulo” – kama ni “kumtukuza hasa”! “Amemtukuza sana” kiasi kwamba, takribani nusu ya Agano Jipya inahusishwa na Paulo! Mtume Petro aliandika vitabu viwili, Mtume Yohana aliandika vitabu vitano; Luka aliandika vitabu viwili, na Yakobo, Mathayo, Marko na Yuda kila mmoja aliandika kitabu kimoja. Mtume Paulo aliandika vitabu 13 vya Biblia, Warumi hadi Filemoni (mwandishi wa kitabu cha Waebrania bado anabishaniwa). Nyaraka za Paulo peke yake zinafanya karibu nusu (13/27 = 48.15%) ya “Agano Jipya” na moja ya tano (13/66 = 19.70%) ya Biblia nzima! Je! Utasema kwamba “Mungu Roho Mtakatifu alimtukuza sana Paulo katika Neno Lake?” Sidhani…!!!

Mwisho wa yote, tunaona katika 1 Wakorintho 3:9-12 kwamba Mtume Paulo ndiye “mkuu wa wajenzi mwenye hekimaaliyeweka msingi na msingi huo ni Yesu Kristo aliyesulubiwa, akazikwa, na kufufuka tena. Hii ni Injili ya Paulo, Injili ya Neema ya Mungu (tazama Matendo 20:24). Petro, Yakobo, na Yohana hawakuwa wajenzi wakuu wenye hekima! Hawakuwa na huduma kwetu sisi watu wa Mataifa na wala Kanisa Mwili wa Kristo (rejea Wagalatia 2:9).

Tunasisitiza tena, Paulo – sio yule mtu, bali ni lile FUNDISHO (the doctrine) lililofunuliwa kipekee kwake, INJILI (the gospel) aliyopewa yeye peke yake na HUDUMA (the ministry) aliyopewa yeye peke yake. Kinyume na mafundisho na tafsiri ya kawaida (jadi) ya Biblia, tunaitambua huduma yake ya kipekee ambayo Bwana Yesu Kristo aliyepaa alimpa Paulo. Bwana alimfunulia Paulo kipekee (peke yake) “ufunuo wa ile siri” (Warumi 16: 25, 26; Waefeso 3:2). Mpango wa Mungu wa wokovu leo ​​unapatikana TU katika nyaraka za Paulo. Baada ya yote, Biblia inasema, “Mungu atahukumu siri za wanadamu na Yesu Kristo kulingana na injili yangu [PAULO]” (Warumi 2:16; linganisha Warumi 16:25; 2 Timotheo 2:8).

Ikiwa imani yako haijajengeka katika uelewa thabiti wa Injili ya Mtume Paulo, Injili ya Neema ya Mungu, ni ukweli ulio wazi, rahisi na usiopingika kwamba uko njiani kwenda kuzimu. Mtu ye yote anayekupenda kwa dhati anahitaji kukuambia ukweli huu mapema kabla ya kitu kingine cho chote katika safari ya wokovu wako. Unahitaji kumtumaini Kristo Yesu peke yako kama Mwokozi wako binafsi leo. Yesu alikupenda na alikufa kwa ajili ya dhambi zako, alizikwa, na akafufuka kwa ajili ya kuhesabiwa haki kwako (1 Wakorintho 15:1-4). Mtumaini Yesu Kristo peke yake, na Mungu atakuokoa milele.

Paulo ni mtume wako na ni mtume wangu, na tunakuwa tunatii muundo wa Mungu pale tunapotumia zaidi ya masomo yetu ya Biblia katika nyaraka za Paulo. HAKUNA CHA ZIADA!

Kwa wale wanaofikiria kwamba sisi tunao uheshimu wito wa Mtume Paulo “tunamtukuza sana Paulo,” pengine wataweza kutafakari upya nafasi zao/imani zao hasa baada ya kuyasoma haya yafuatayo:

  1. Je! Unaweza kuelezea kabisa mpango wa Mungu wa wokovu (kifo, kuzikwa, na kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo kama malipo kamili ya dhambi zetu), bila kutaja hata moja ya aya yoyote inayopatikana kati ya vitabu vya Paulo (Warumi mpaka Filemoni)? – Hutaweza, kwa sababu unahitaji nyaraka za Paulo kuelezea Injili ya Neema ya Mungu – injili ya kipindi hiki (1 Wakorintho 15:3-4) – hii inapatikana tu katika nyaraka za Paulo!).
  2. Je! Bila ya kutumia nyaraka za Paulo (Warumi mpaka Filemoni), unaweza kuelezea maana ya Kanisa (Mwili wa Kristo) na unyakuo kwa usahihi? Je! Tunapaswa kuishije kama waumini wa Kristo katika kipindi hiki? Je! Tupo chini ya sheria au neema? Je! Ni nini kusudi na hatima ya Kanisa Mwili wa Kristo? Huwezi kujibu maswali haya nje ya nyaraka za Paulo.
  3. Je! Unaweza kuniambia juu ya utaratibu wa kanisa – church order (sifa za maaskofu, mashemasi, n.k.) bila kutumia vitabu vya 1 na 2 Timotheo na Tito?
  4. Je! Unaweza kuelezea taifa la Israeli liko wapi leo? Je! Sisi ni Israeli wa kiroho? Je! Mungu atarudi kushughulika na Israeli siku za usoni? Unaweza kujibu tu maswali haya kwa kutumia nyaraka za Paulo.
  5. Je! Unawezaje kusema “nimeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani” bila Paulo? – Fundisho hilo umelitoa wapi? – Sijui kama unajua kwamba, Yesu Kristo wala Mtume Petro hawakuwahi kusema hivyo!

HAKIKA HUTAWEZA!

Bila nyaraka za Mtume Paulo, huwezi kufanya lo lote kati ya hayo hapo juu. Kama ndivyo, nawe pia – HAKIKA “UNAMTUKUZA SANA PAULO”!

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *