1 |
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; |
2 |
ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; |
3 |
hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele. |
4 |
Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara. |
5 |
Na katika wana wa Lawi nao, wale waupatao ukuhani, wana amri kutwaa sehemu ya kumi kwa watu wao, yaani, ndugu zao, kwa agizo la sheria, ijapokuwa wametoka katika viuno vya Ibrahimu. |
6 |
Bali yeye, ambaye uzazi wake haukuhesabiwa kuwa umetoka kwa hao, alitwaa sehemu ya kumi kwa Ibrahimu, akambariki yeye aliye na ile ahadi. |
7 |
Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa. |
8 |
Na hapa wanadamu wapatikanao na kufa hutwaa sehemu ya kumi; bali huko yeye ashuhudiwaye kwamba yu hai. |
9 |
Tena yaweza kusemwa ya kuwa, kwa njia ya Ibrahimu, hata Lawi apokeaye sehemu ya kumi alitoa sehemu ya kumi; |
10 |
kwa maana alikuwa katika viuno vya baba yake, hapo Melkizedeki alipokutana naye. |
11 |
Basi, kama ukamilifu ulikuwapo kwa ukuhani wa Lawi; (maana watu wale waliipata sheria kwa huo); kulikuwa na haja gani tena ya kuhani mwingine ainuke, kwa mfano wa Melkizedeki, wala asihesabiwe kwa mfano wa Haruni? |
12 |
Maana ukuhani ule ukibadilika, hapana budi sheria nayo ibadilike. |
13 |
Maana yeye aliyenenwa hayo alikuwa mshirika wa kabila nyingine, ambayo hapana mtu wa kabila hiyo aliyeihudumia madhabahu. |
14 |
Maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika Yuda, kabila ambayo Musa hakunena neno lo lote juu yake katika mambo ya ukuhani. |
15 |
Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki; |
16 |
asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo; |
17 |
maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki. |
18 |
Maana, kuna kubatiliwa kwa ile amri iliyotangulia, kwa sababu ya udhaifu wake, na kutokufaa kwake; |
19 |
(kwa maana ile sheria haikukamilisha neno); na pamoja na hayo kuliingizwa matumaini yaliyo mazuri zaidi, ambayo kwa hayo twamkaribia Mungu. |
20 |
Na kwa kuwa haikuwa pasipo kiapo, |
21 |
(maana wale walifanywa makuhani pasipo kiapo; bali yeye, pamoja na kiapo, kwa yeye aliyemwambia, Bwana ameapa wala hataghairi, Wewe u kuhani wa milele;) |
22 |
basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. |
23 |
Tena wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na mauti wasikae; |
24 |
bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. |
25 |
Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. |
26 |
Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; |
27 |
ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. |
28 |
Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele. |
Leave a Reply