Home 2020 March 06 Wanafunzi wa Yesu Hawakuhubiri Msalaba kwa Ajili ya Wokovu

Wanafunzi wa Yesu Hawakuhubiri Msalaba kwa Ajili ya Wokovu

Wanafunzi wa Yesu Hawakuhubiri Msalaba kwa Ajili ya Wokovu

Ni dhahiri kutoka 1 Wakorintho 15:1-4 kwamba injili ya wokovu wetu inajumuisha kifo, kuzikwa, na kufufuka kwa Yesu kama malipo ya dhambi zetu. Ukweli huu rahisi, ni msingi wa Ukristo. Hata hivyo, hakuna sehemu yoyote katika vitabu ya Mathayo, Marko, Luka, au Yohana ambapo wanafunzi wale kumi na wawili wa Yesu (Thenashara) walielewa kuhubiriwa kwa msalaba. Ifuatayo, hapa chini, ni mistari inayothibitisha kuwa wale kumi na wawili walikuwa ni ‘wajinga’ wa kuhuhubiriwa kwa msalaba kwa ajili ya wokovu.

A: Walikuwa ‘wajinga’ wa kifo, kuzikwa, na ufufuko wa Yesu
Mathayo 16:21-22, Yesu kwa mara ya kwanza alianza kuwaambia wanafunzi wake juu ya kifo chake na bado Petro alijaribu kumzuia, tena kwa kumkemea!
Marko 8:31-32, Taarifa nyingine juu ya Petro kumkemea Bwana kwa sababu ya kuzungumza kuhusu kifo chake.
Marko 9:31-32, Pamoja na kusikia kuhusu kifo na ufufuko wa Yesu, wanafunzi hao wa Yesu “hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza
Luka 9:44-45, “Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile”
Luka 18:31-34, “Akawachukua wale Thenashara, akawaambia, Tazameni, tunapanda kwenda Yerusalemu, na mambo yote yatatimizwa, Mwana wa Adamu aliyoandikiwa na manabii. Kwa kuwa atatiwa mikononi mwa Mataifa, atafanyiwa dhihaka; atatendwa jeuri, na kutemewa mate; nao watampiga mijeledi, kisha watamwua; na siku ya tatu atafufuka. Walakini hawakuelewa maneno hayo hata kidogo, na jambo hilo lilikuwa limefichwa kwao, wala hawakufahamu yaliyonenwa
Yohana 2:21-22, Hawakuelewa ufufuko wa Yesu mpaka baada ya kutokea!

B: Hawakusadiki kuwa Yesu alifufuka!
Marko 16:5-14, Wanawake walikuwa na hofu wakati walipoliona kaburi likiwa tupu. Wanafunzi wake hawakusadiki habari hizo, hata baada ya mashahidi wawili kuwashuhudia (kuwadhibitishia) juu ya habari za ufufuko huo. Yesu alipojidhihirisha kwao, aliwakemea kwa kutokuamini kwao na kwa ugumu wa mioyo yao!
Luka 24:1-4, Wanawake walifadhaishwa kwa sababu ya kile kilichomtokea Yesu, kaburi lake lilikuwa wazi!
Luka 24:8-12, Habari za Yesu kufufuka zilionekana kuwa ni UPUZI kwa wanafunzi!
Yohana 20:2, Mariamu Magdalene aliamini kwamba ‘Bwana aliondolewa kaburini’, akidhani kwamba kuna watu (wabaya) walikuja kuondoa jiwa kaburini alimozikwa na kuondoka na ‘mwili’ wake.
Yohana 20:7-10, Wanafunzi nao baada ya kuona kaburi liko wazi, waliziamini habari za Mariamu kwamba ‘Bwana aliondolewa kaburini’ na wakaondoka zao. Hawakujua chochote kuhusu kufufuka kwa Yesu!

C: Hawakutambua kazi ya msalaba hata baada ya ufufuko
Yohana 20:21-23, Hata baada ya Yesu kufufuka, wanafunzi wake hawakufahamu nini kimekamilishwa na msalaba huo. Hapa, wanafunzi hao, wanapewa mamlaka ya kusamehe dhambi!
Matendo 3:14-15, Habari za kusulubiwa kwa Yesu zilitolewa kama mashitaka ya mauaji kwa taifa la Israeli katika siku ile ya Pentekoste. Habari za ufufuko nazo zilitolewa kama ‘onyo’ kwamba Mungu atarudi kufanya kisasi.
Matendo 5:28, Badala ya damu ya Yesu Kristo kuwa malipo kamili/tosha ya dhambi, ilionyeshwa/ilihubiriwa kama ushahidi wa wauaji wenye hatia.
Matendo 7:52, Stephen anawatuhumu watawala kwa usaliti wao na mauaji ya mtu Mwenye Haki.
Matendo 10:39, Kulingana na injili ya Paulo Kristo alikufa kwa hiari yake kuchukua nafasi ya wenye dhambi. LAKINI, kulingana na Petro, Kristo alikufa kwa sababu aliuawa na baadhi ya Wayahudi. Je, haupo uwezekano kwamba Petro alikuwa haelewi bado SIRI YA MSALABA?

Orodha hii haithibitishi kwamba wale wanafunzi kumi na wawili hawakuwa watiifu kwa injili ambayo iliwasilishwa kwao. Lakini kinyume chake, hakika wao walikuwa ndio waumini wa kwanza katika injili ya ufalme. Wao walikuwa kati ya kundi (sazo) aminifu katika Israeli ambao walioamini kwamba Yesu alikuwa Mwana wa Mungu na Masihi aliyehaidiwa.
Hata hivyo, mistari hii inaonyesha kwamba injili waliyoijua na kuiaminiwa HAIKUWA kuhubiriwa kwa msalaba ambayo Paulo aliifundisha. Wakati wao walimjua Yesu Kristo kama Masihi kwa Israeli, Paulo baadae aliweza kufundisha kuwa Yesu Kristo, juu ya msalaba, alifanyika kuwa malipo ya dhambi kwa watu wa Mataifa.
Kuhubiriwa kwa msalaba kulitolewa, mara ya kwanza, kwa ajili ya wokovu kupitia kwa Mtume Paulo kama Bwana alivyomfunulia maana ya kufa, kuzikwa na kufufuka kwake. Wale Mitume kumi na wawili walikuwa ‘wajinga’ wa SIRI HII.

Author: Festus Patta

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *